Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Mungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa leo mapema asubuhi tarehe 27.11.2021 ameweka jiwe la msingi ujenzi wa vyumba vinne vya madarasa katika shule ya sekondari Wasichana Kayuki.
Ujenzi huo unaotekelezwa chini ya mpango wa UVIKO 19 unazinufaisha shule 18 za sekondari kwa ujenzi wa vyumba vya madarasa 55 na utagharimu shilingi billion 1.1 fedha iliyotolewa na Serikali kuu.
Akiwa katika shule ya sekondari kayuki Mhe. Majaliwa ameipongeza Halmashauri ya wilaya ya Rungwe kwa kutekeleza ujenzi huu kwa zaidi ya asilimia 50% katika shule zote 18 na kuwa kwa kufanya hivi wanafunzi wote waliochaguliwa kujiunga kidato cha Kwanza wataanza masomo yao mapema mwakani.
'Kiujumla niipongeze Halmashauri hii kwa kazi kubwa ya ujenzi iliyofanyika madarasa yamejengwa kwa viwango, mafundi ninawaona wanajituma na nimeambiwa wanafanya kazi usiku na mchana. Hongereni sana. Ameongeza.
Aidha ameagiza vyumba vyote vya madarasa kukamilika ifikapo Disemba 10 mwaka huu katika wilaya nzima siku tano kabla ya tarehe ya kitaifa kufikia ukomo.
Hata hivyo Mhe. Majaliwa amemuagiza Naibu Katibu Mkuu TAMISEMI anayeshughulikia elimu Bwana Gerald Mweli kuhakikisha anaiweka shule ya sekondari Kayuki katika Mpango wa ukarabati wa Majengo na miundombinu yake ili kusaidia kuongeza ufaulu shuleni hapo.
"Wanafunzi wangu mnapendeza sana, na pia ufaulu wenu darasani ni Mzuri mno hivyo nikuagize Naibu Katibu Mkuu uende wizarani na kuiweka shule hii katika mpango wa Ukarabati Mkubwa kwani nimezunguka huko nyuma hali si nzuri sana" amesisitiza
Kuhusu sehemu ya ardhi iliyotolewa na kampuni ya Mohamedi Enteprises kwa shule hiyo, Mhe. Waziri Mkuu ameahidi kuwasiliana na kampuni hiyo ili itoe mapema kipande hicho cha ardhi zaidi ya ekari 10 ili zisadie kupanua miundombinu ya elimu shuleni hapo.
Katika hatua nyingine Mhe. Waziri Mkuu ameweka jiwe la msingi ujenzi wa jengo la maktaba katika chuo cha ualimu Tukuyu unaotarajia kugharimu zaidi ya shilingi million 300 huku akiagiza watumishi kote nchini kufanya kazi kwa bidìi na hivyo kuleta matokeo chanya kwa jamii.
Pamoja na kufanya ziara maeneo ya elimu,Waziri mkuu pia amehitimisha ziara yake Wilayani Rungwe kwa kutembelea kiwanda cha kuzalisha maji ya kunywa cha Tukuyu spring water kilichopo kijiji cha Kibisi kata ya Kyimo na kushukuru uongozi wa kiwanda hicho kwa kuongeza ajira kwa vijana, kusambaza umeme kwa kaya jirani, kusambaza maji ya bomba kwa wananchi, kutoa vifaa vya ujenzi shule mpya ya sekondari KIBISI sambamba na kuwa mlipaji mzuri wa kodi ya serikali.
Tukuyu Mjini-Mkabala na Benki ya NMB
Sanduku la Posta: Box 148
Simu: 025 255 2586
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: ded@rungwedc.go.tz
Haki Miliki ©2021 GWF. Haki Zimehifadhiwa