Wananchi wa Kata ya Ikuti walitoa kero zao kwa Mkurungenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Rungwe Bibi Loema I. Peter alipokuwa katika mkutano wa hadhara wa kusikiliza kero za Wananchi, uliofanyika tarehe 10/07/2018 katika viwanja vya kituo cha Afya Ikuti. Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Rungwe aliongozana na Wakuu wa Idara ambao ndiyo wasaidizi wake kiutendaji. Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Rungwe kwa kushirikiana na wakuu wa idara walijibu kero hizo kwa wananchi na kutolea ufafanuzi wa malalamio yaliyotolewa katika mkutano huo wa hadhara.
Baadhi ya kero ambazo zilisikilizwa ni pamoja na Faini kwa akina mama wanaojifungulia majumbani, ukosefu wa huduma ya maji na umeme, kukosekana kwa baadhi ya dawa kwa huduma ya Bima ya Afya pamoja na ukosefu wa Walimu wa Sayansi katika Kata hiyo.
Kaimu Mhandisi wa Maji ndugu Moses Mwalisatile alipokua akijibu kero ya ukosefu wa huduma ya maji kwa baadhi ya maeneo ya vijiji vya Kata hiyo alisema kwamba, changamoto kubwa iliyosababisha ukosefu wa huduma ya maji maeneo hayo ni wananchi kutokuwa na ushirikiano wa kutosha kusaidia katika kusambaza miundo mbinu ya maji ikiwa ni pamoja na kusaidia kuchimba mitaro, hivyo Idara ya maji ilishindwa kusambaza huduma hiyo kwa wakati. Aidha Kaimu Muhandisi wa Maji alieleza kuwa Idara ya Maji imejipanga kuendelea na kusambaza huduma ya upatikanaji maji kwa kuongeza vyanzo vya maji ikiwa ni kutoa majia katika chanzo cha milima ya Isugha iliyopo katika Kata hiyo. Mkurugenzi Mtendajio wa Halmashauri ya Wilaya ya Rungwe aliwataka wananchi wa Kata hiyo kutoa ushirikiano katika kazi za usambazaji huduma ya maji ili kutekeleza kauli mbiu ya "kumtua mama ndoo kichwani''. Pia aliwasisisitiza kushiriki vema katika kazi za maendeleo maana jamii ina wajibu wa kushirikiana na Serikali katika kuleta maendeleo katika jamii husika na Taifa kwa ujumla.
Wakina mama wanao jifungulia majumbani kutozwa faini ni kero iliyojibiwa na Kaimu Mganga Mkuu wa Wilaya ya Rungwe Bi. Adelina Alfred alisema kwamba; faini wanazotozwa akina Mama wanaojifungulia majumbani au kwa Wakungawa jadi ni adhabu ya kukomesha vitendo hivyo ambavyo husababisha vifo vya Mama na Mtoto. Kamati ya Maendeleo ya Kata (KAMAKA) ilipanga adhabu hiyo baada ya Mganga Mkuu wa Kituo cha Ikuti kutoa taarifa ya ongezeko la vifo vya Mama wajawazito na Watoto wachanga. Kaimu Mganga Mkuu wa Wilaya aliwashauri Mama wajawazito kwa kushirikiana na waume zao wahudhdurie Kliniki kwa ajili ya kupata huduma zinazotakiwa, piwa aliwataka kuacha kujifungulia majumbani na kwa Wakunga wa Jadi na badala yake waende kujifungulia Kituo cha Afya.
Aidha Kaimu Mganga Mkuu aliwapa elimu wananchi juu ya dawa zinazotolewa kwa Bima ya Afya kuwa; zinatolewa kulingana na kiwango cha Kituo cha Afya (Level) hivyo si dawa zote zinapatikana kwa kila kituo cha afya.
Kaimu Afisa Maendeleo ya Jamii Wilaya Bi.Bhoke Anderson alijibu kero ya wananchi ya Wanawake na Vijana wa Kata hiyo ya kutopata mikopo inayotolewa na Halmashauri ya Wilaya ya Rungwe kila baada ya miezi mitatu kuwa, kwa mwaka wa fedha 2017/2018 hakuna kikundi chochote kilichoomba mkopo kutoka Kata ya Ikuti. Kikundi kilichokua kimeomba mkopo kwa mwaka wa fedha 2016/2017 walimaliza kulipa mkopo huo na hawakuomba tena hivyo aliwashauri vikundi vya wanawake,vijana na walemavu ambao vikundi vyao vina usajili waombe mikopo na Idara ya Maendeleo ya Jamii kwa kuzingatia vikundi vitakavyokidhi vigezo na masharti vitapata mikopo hiyo.
Ukosefu wa walimu wa sayansi ni kero iliyojibiwa na Kaimu Afisa Elimu Sekondari Ndugu Auckland Hyera kwa kueleza kwamba shule ya sekondari Ikuti inawalimu wa sayansi wa kutosha kwa kuzingatia idadi ya mikondo kwa kila darasa na idadi ya wanafunzi. Aidha alieleza kuwa, pindi Serikali itakapoajiri Walimu wapya wa masomo ya Sayansi, Shule ya Sekondari Ikuti itaongezewa idadi ya Walimu wa masomo hayo.
Shule ya Sekondari Ikuti, ni miongoni mwa shule za Sekondari wilayani Rungwe zilizofanya vizuri katika ufaulu wa masomo ya Sayansi kwa Kidato cha IV 2017.
Tukuyu Mjini-Mkabala na Benki ya NMB
Sanduku la Posta: Box 148
Simu: 025 255 2586
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: ded@rungwedc.go.tz
Haki Miliki ©2021 GWF. Haki Zimehifadhiwa