WAKAZI WA KATA YA LUFINGO WANUFAIKA NA BARABARA YA LAMI
Mkuu wa Wilaya ya Rungwe Mhe.Jaffar Haniu amezindua leo tarehe 24.8.2023 ujenzi wa barabara ya Ndulilo mpaka Itete kwa Kiwango cha Lami inayounganisha kata ya LUFINGO na KYIMO yenye umbali wa KM 11.38 kwa gharama ya shilingi Billion 8.9
Akizindua barabara hiyo Mhe.Haniu amempongeza Mhe Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kutoa kiasi hicho cha fedha na kuwa inaenda kufungua fursa za kiuchumi sambamba na usafirishaji wa watu na mali zao.
Amesema Serikali imeendelea kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo ikilenga kuwaondolea changamoto mbalimbali Wananchi ikiwemo usafirishaji, elimu, afya, maji na umeme.
" Leo tunashuhudia uzinduzi wa barabara hizi lakini vituo vya afya, madarasa pamoja na maji yanasambazwa kwa kasi huko vijijini na hizi ni juhudi za serikali yenu tukufu inayoongozwa na Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan" Ameongeza.
Aidha amewaomba wananchi kutoa ushirikiano kwa Mkandarasi anayetekeleza mradi huo na kujiepusha na vitendo vinavyoweza kurudisha nyuma maendeleo ya mradi ikiwemo vitendo vya uwizi wa vifaa vya ujenzi.
Katika hatua nyingine Mheshimiwa Haniu ametoa rai kwa wananchi kutojitokeza na kuomba fidia dhidi ya mradi na kuwa vikao vilishafanyika huko nyuma na wananchi kuridhia kuondoa mazao yao bila kufidiwa chochote.
Naye Mwenyekiti wa Chama chama cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Rungwe Ndugu Mekson Mwakipunga ameishukuru serikali kwa kutekeleza Ilani ya Chama Tawala na kumuomba Mkandarasi kutoa ajira kwa wazawa hatua itakayoongoza kipato na hivyo kuboresha maisha ya wananchi.
Wakati huohuo Wakazi wa kata hiyo wameishukuru Serikali kwa kuwajengea barabara hiyo.
Joseph Mwakasungura Mkazi wa kijiji cha Kali ameipongeza Serikali kwa hatua hiyo na kuwa itarahisisha usafirishaji wa mazao ya ndizi , Kahawa, maziwa, pamoja na parachihi kutoka Shambani Kuelekea sokoni.
Naye Ana Aswile Mkazi wa kijiji cha Lufingo ameshukuru ujenzi huo na kuwa itawarahishia Kufika kwa urahisi katika vituo vya kutolea huduma ya afya hasa kwa Mama Wajawazito.
Barabara hiii inayojengwa na kampuni ya Sigh&Sons Company kutoka mkoa wa Kilimanjaro , chini ya Usimamizi wa Wakala wa Barabara Mjini na Vijijini (TARURA), inafadhiriwa na Mradi wa Agri-Connect na inatarajia kukamilika baada ya Mwaka mmoja kuanzia tarehe 01.9.2023
Tukuyu Mjini-Mkabala na Benki ya NMB
Sanduku la Posta: Box 148
Simu: 025 255 2586
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: ded@rungwedc.go.tz
Haki Miliki ©2021 GWF. Haki Zimehifadhiwa