Noah kibona, Rungwe Dc
“Kutokujua si kosa shida ni kutofuatilia baada ya kujulishwa” haya ni maneno yaliyosemwa na mtalaamu wa falsafa na saikolojia Emil Durkhem (1890) wakati anajaribu kuelezea binadamu na uwezo wake kupuuza mambo ya msingi katika jamii.
Wilaya ya Rungwe mkoani Mbeya ni moja ya wilaya nchini Tanzania amabayo imejaliwa kuwa na fursa nyingi za kiuchumi ambazo kwa muda mrefu zimesaidia kuboresha maisha ya jamii kwa ngazi ya kaya na mtu mmoja mmoja kwa ujumla. Hali ya hewa kuwa ya mvua nyingi na joto la wastani pamoja udongo wenye rutuba unafanya mazao mengi kustawi bila shida. Wageni karibuni Rungwe!
Uwekezaji mpya katika kilimo sasa umebebwa na zao la Vanilla ambalo limeanza kulimwa karibu kona zote ndani ya Halmashauri ya wilaya ya Rungwe na kaya nyingi zimeanza kulichangamkia kwa kuwa ni zao amabalo halihitaji eneo kubwa sana na linaweza kuchanganywa ndani ya mazao mengine (intercropping).
UKUUAJI WA ZAO VANILA
Zao la Vanilla hustawi katika joto kati ya sentigredi 25-35 na mwinuko upatao mita 1000 hadi 1500. Pia hustawi zaidi katika eneo linalopata mvua kati ya mililita 2500 mpaka 5000 na huhitaji miezi miwili ya kiangazi ili kuruhusu maua kuchanua. Mizizi yake husambaa juu ya udongo uliosheheni mbolea ya mboji.
Zao la vanilla hutambaa kama tambazi hivyo vipando vyake husiwa ardhini na kisha kuning’inizwa kwenye mti ambao hubeba shina zima la vanilla. Mti unaobeba shina la vanilla lazima uwe umeoteshwa ili kuepuka kuoza na kudumu kwa muda mrefu.
Miti kama kisamvu mpira na mibono hutumika zaidi kwa kuwa huchipua mapema zaidi. Wataalamu wanashauri kuwa kiwatilifu cha mkojo wa ng’ombe kimependekezwa kuua wadudu wasumbufu ambapo mkojo huo huhifadhiwa kwenye chupa ya lita tano kwa siku 14 na kisha kuchanganywa kwenye pampu ya lita 20 tayari kwa upuliziaji.
Kwa misingi ya kilimo hai inashauriwa kutumia samadi na maozea mbalimbali ya mimea ili kurutubisha ardhi. Vanilla huzalisha matunda yanayo fanania na maharagwe na urefu wake huwakati ya sentimita 10-25 cm. Mmea huu huweza kukua na kufikia urefu wa mita 15 hadi 20. Maua yake huwa makubwa ,manene na hunukia na yana rangi ya kijani isiyo kolea pamoja na njano.
UPATIKANAJI WA MICHE/VIPANDO VYA VANILA
Zao la vanilla ni geni katika wilaya ya Rungwe hivyo hata upatikanaji wake hutegemea uwezeshaji kutoka maeneo mengine. Pamoja na kwamba Kagera ndio mkoa pekee unaozalisha kwa wingi matunda ya vanilla lakini inashauriwa kuagiza kutoka nchini Uganda kwa kuwa ugonjwa wa mnyauko wa migomba umeenea mkoani Kagera hinyo uletaji vipando vyake wilayani Rungwe ungeathiri Migomba kwa kuwa zao la vanilla hulimwa kwa kuchanganywa na Migomba na mimea mingine rafiki.
SOKO LA VANILA
Bwana Juma Mzala ni mtaalamu wa Kilimo wilaya ya Rungwe na anabainisha kuwa Vanilla huuzwa sana katika nchi za Ulaya na Marekani ambapo kwa sasa bei ya kilo moja hapa nchini ni kati ya shilingi 100,000/= hadi 150,000/=. Aidha bwana Mzala anabainisha kuwa mpaka sasa zaidi ya miche 61,000 imepandwa na lengo ni kuwafikia wakulima wapato 600 kwa mwaka huu ambapo inakisiwa kuwa idadi hiyo ya wakulima itaweza kuzalisha tani 222.5 sawa na zaidi ya shilingi billion 22 zitakazopatikana baada ya mauzo na hivyo wakulima kuondokana na lindi la umasikini.
MATUMIZI YA VANILLA
Vanilla ni kiungo ghali sana duniani baada ya zao la Safron amabalo hulimwa sana katika nchi za Asia. Vanilla hutumika kama kiungo kwenye chakula kwa ajili ya kuongeza radha na lishe katika mwili wa binadamu. Pia hutumika kutengenezea keki, maandazi,biskuti,barafu, uji, chokoleti na vinywaji mbalimbali ikiwa ni pamoja na yorgut, soda na juice.
MTANDAO WA VANILA WILAYANI RUNGWE
Bwana Mzala anabainisha kuwa Mpaka sasa katika Wilaya ya Rungwe baadhi ya kata zimeanza kulima zao hili ikiwemo kata ya KIWIRA, KYIMO, BAGAMOYO, IBIGI, MPUGUSO, KISONDELA, NKUNGA, KINYALA, LUPEPO na zingine kadhaa. Mwitikio mkubwa umeonekana katika kata ya kiwira na Kyimo ambapo zaidi ya wakulima 100 wamenufaika.
Bwana Andrew Mwike ni mkulima katika kijiji cha Kisondela na anbainisha kuwa kwa sasa amebahatika kupanda vipando vipatayo miamoja katika kiunga kidogo cha shamba lake huku akiahidi kuongeza zaidi vipando vingi na kuendelea kuwahamasisha wakulima zaidi kujihusisha na kilimo cha vanilla. “Mimi nimeanza kilimo cha vanilla kwa kupanda vipando 50 lakini nikahamasika kuongeza vingine 50 na kwa sasa ninauhakika kupata mazao mengi na nitaandaa semina niwahamasishe wenzangu makanisani hata mikutano ya hadhara” alisisitiza.
Zao hili limewafurahisha wakazi wengi wilayani Rungwe, kutokana na uhaba wa ardhi sasa wanaweza kuchanganya na mazao mengine kama kahawa, migomba, Chai na mazao mengine ya misitu. Mchungaji Anyigulile Kasake anaiona fursa hii kwa kuwa ana ekari mbili tu za migomba na sasa ataweza kutumia sehemu ya shamba lake kupanda Vanilla huku akitarajia kuvuna zaidi ya kilo 200 ambazo zitamletea kipato kikubwa na kumuwezesha kujenga nyumba bora na kununua shamba kubwa zaidi.
Mchungaji Kasake ambaye pia ni mkazi wa Kata ya Kyimo imejikusanyia wakulima wengi wa Vanila wakiwemo waumini wake ambapo kwa kushirikiana sasa wameanzisha Shamba darasa ambalo sasa linatumika kufundishia wakulima wengine.
Afisa kilimo bwana Mzala anaunga mkono mshikamano huu na kushauri maafisa ugani walio karibu yao kueendelea kuwapa ushauri wa karibu ili kuriboresha zao hili.
Mahitaji sasa yanazidi kuongezeka kwa wakulima wengi kujitokeza kulima zao hili amabapo wakulima wanashauriwa kuwaona maafisa ugani walio karibu nao na pia kufika ofisi za kilimo ili kupata mbinu bora za kupanda na kuendeleza zao la vanilla ili kuhimili soko la ushindani kwa kuzalisha matunda yenye ubora.
Bwana Mzala anasisitiza kuwa wanunuzi wa zao hili wapo tayari na Kampuni ya Natural Extract Industry kutoka mkoani Kilimanjaro imejitokeza kununua matunda hayo mara Msimu utakapo wadia.
UTALII WA KILIMO KUONGEZEKA WILAYANI RUNGWE
Utalii wa namna hii waweza kuwa mgeni miungoni mwa wakazi wa wilaya ya Rungwe. Katika hali isiyo ya kawaida wapo watu tangu wazaliwe hawajawahi kuona mmea wa Chai, Parachichi, na hata kahawa. Sasa zao la Vanilla.
Wageni wengi hupenda kuja kuona muonekano, upandaji na uendelezaji wa mazao haya na wakati mwingine mashamba makubwa (Estate farm) yenye rangi ya kijani na hewa safi.
Wanapokuja ni lazima watoe nauli au kununua mafuta kugharimia safari yao, pia ni lazima wale chakula na kupata malazi na wakati mwingine kutibiwa katika maeneo yetu.
Hii huongeza pato kubwa katika Wilaya yetu kwa mtu mmojammoja na jamii yote kwa ujumla. Fursa hii inaweza kuchangamkiwa kwa wakazi sasa kuanza kuboresha kilimo chao ili wakazi wa maeneo mengine waone ndio eneo pekee la kuboresha ufahamu wao katika kilimo na faida nyigine kadha wa kadha.
Tukuyu Mjini-Mkabala na Benki ya NMB
Sanduku la Posta: Box 148
Simu: 025 255 2586
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: ded@rungwedc.go.tz
Haki Miliki ©2021 GWF. Haki Zimehifadhiwa