Noah kibona Rungwe Dc.
Imeelezwa kuwa uzingatiaji sahihi wa lishe katika ngazi ya kaya huchochea ustawi bora wa jamii ikiwemo ukuaji wa ubongo na afya ya mwili.
Rai hiyo imetolewa na Mkuu wa Wilaya ya Rungwe Mh. Chalya Julius Nyangidu wakati akifungua kikao kazi cha afua za lishe ambacho pamoja na mambo mengine kilisisitiza jamii kuzingatia chakula chenye viini lishe.
Mh. Chalya ambaye kitaluma ni mtaalamu wa kilimo na mifugo alisisitiza kuwa pamoja na Wilaya ya Rungwe kuwa na vyakula vingi mchanganyiko lakini bado kiwango cha utapiamulo kwa watoto na watu wazima kipo kwa kiwango cha juu ili hali mbinu za kuepukana na kadhia hii zipo na zinaweza kufuatwa iwapo tu wananchi watabadili mifumo ya ulaji wa chakula.
Aidha Mh Chalya aliwasihi wakazi wa Wilaya ya Rungwe kula vyakula mchanganyiko huku akiacha nasaha kuwa kula ndizi changa ambazo hazijakomaa ni bora zaidi kwani zina viini lishe zaidi ya ziliyokomaa sana.
Akitoa nukuu mbalimbali Mh. Chalya aliomba watanzania wote kuzingatia mbinu za usalama wa chakula ambazo ni pamoja na kukitafuta chakula kwa kulima au kununua, kukiandaa na kukitunza kulingana na mahitaji na kuweka bajeti ili kisiishe na kuepuka na baa la njaa na kusisitiza kuwa elimu hii lazima isambazwe mashuleni, nyumba za ibada na mikutano ya hadhara.
Pamoja na hayo afisa lishe halmashauri ya Wilaya ya Rungwe Bi. Halima Kameta aliongeza kuwa wilaya ya Rungwe inakadiriwa kuwa na watoto wapatao 47800 na kati ya hao watoto 576 wana udumavu baada ya kukosa lishe stahiki ambapo mpaka sasa kampeni zinaendelea kwa kupima hali ya utapiamlo ikiwemo huduma ya matone na chanjo mbalimbali.
Hata hivyo akitoa takwimu zaidi afisa lishe mkoa wa Mbeya bwana Benson Sanga alisema kuwa kwa sasa udumavu kimkoa umepungua ambapo mwaka 1991 ulikadiriwa kufikia asilimia 50 na mwaka 2018 umepungua kufikia asilimia 32 hali inayotia moyo na kupunguza tishio la kupata watoto wenye uwezo mdogo wa kufikiri, kukosa umakini na zaidi akina mama kupata shida wakati ya kujifungua na kupata watoto wenye ulamavu akitolea mfano ugonjwa wa mgongo wazi na vichwa vikubwa.
Akisisitiza zaidi bwana Sanga alitoa sababu za utapiamulo kuwa ni pamoja na ulaji duni wa chakula, kukosa uchangamshi kwa kucheza michezo mbalimbali na magonjwa ya mara kwa mara kuwa hupelekea taifa la watu wasioelimika pamoja na kupata viongozi wasiofikiri na hivyo kupoteza nguvu kazi hasa katika falsafa tuliyonayo sasa ya taifa la viwanda.
Akifunga kikao kazi hicho kaimu Mwenyekiti wa halmashauri ya Wilaya ya Rungwe Mh. Emmanuel Mwaijande aliomba idara ya elimu ,kilimo, afya na maendeleo ya jamii kuhakikisha inawahamasisha wananchi kuzingatia mlo kamili na kupata matibabu mara kwa mara ili kupunguza jamii yenye udumavu.
Tukuyu Mjini-Mkabala na Benki ya NMB
Sanduku la Posta: Box 148
Simu: 025 255 2586
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: ded@rungwedc.go.tz
Haki Miliki ©2021 GWF. Haki Zimehifadhiwa