TEMBEA NA WATU UVAE VIATU
Mwanzoni mwa mwaka 1960 baada ya uhuru na nchi kupitia kipindi kigumu cha uchumi (economic crisis) mwaka 1980 usemi huu ulikuwa maarufu sana.
Fuatana nami katika makala hii fupi nikuvalishe viatu kupitia kiwanda cha utengenezaji bidhaa za ngozi kilichopo kata ya Bulyaga nyuma ya shule ya msingi Madaraka karibu na ofisi ya mtendaji wa kata.
Hawa ni vijana. Ni Vijana kwelikweli walioamua kuungana pamoja kuakisi methali ya umoja ni nguvu utengano ni udhaifu huku wakijumuisha maarifa yao kupambana na umasikini.
Kikundi cha vijana BAM Investiment kilichoasisiwa na kusajiliwa rasmi mwaka 2020 kikiwa na wanachama 8 kililenga kuzalisha ajira zaidi kwa vijana ikiwa ni pamoja na kutoa mafunzo ya ujasiriamali.
Baraka Mwampulule ndiye kiongozi wa kikundi hiki ambapo mbele ya kamati ya siasa wilaya ya Rungwe ametaja shughuli zinazotekelezwa na kikundi hiki kuwa ni pamoja na uzalishaji bidhaa za ngozi kama viatu,mikoba, pochi, waleti na viatu vya wazi "sandals". Shughuli nyingine ni ufugaji wa nguruwe na upambaji wa kumbi za starehe.
Bwana Mwampule anaongeza kuwa kikundi kilianza na mtaji wa shilingi 750,000/= ikiwa ni michango ya wanachama hadi kufikia shilingi million 2 mtaji uliosaidia kununua mashine za uzalishaji sambamba na ununuzi wa malighafi.
"Mtaji huu ulitusaidia sana tukaanza kuzalisha bidhaa za ngozi ikiwa ni sehemu ya kujitambulisha kwa jamii huku tukilenga kupanuka zaidi" ameongeza bwana Mwampulule.
Kikundi hiki kiliendelea kupanuka na kuanza kuzalisha bidhaa bora na zenye tija kwa watumiaji na hivyo kupanua wigo wa mahitaji kwa wateja.
HALMASHAURI YAWASHIKA MKONO
Serikali kupitia Halmashauri ya wilaya ya Rungwe katika mwaka wake wa fedha 2020/21 kilizibaini juhudi zinazofanywa na kikundi hiki na kukipatia mkopo wenye thamani ya shilingi million 10 ili kuunga mkono jitihada zinazofanyika na hivyo kuongeza ajira kwa vijana wengi zaidi.
Aidha Halmashauri ilikipatia kikundi machine mpya ya kuundia bidhaa za ngozi hali iliyokiwezesha kuzalisha zaidi ya jozi 40 za viatu na zingine kwa uwingi zaidi na hivyo kuliteka soko katika wilaya ya Rungwe.
Ikilenga kuongeza uzalishaji na kupata eneo bora la kutoa mafunzo kwa vijana wengi zaidi, Halmashauri pia ilitoa jengo ambalo mpaka sasa kikundi hicho kinaendelea kulitumia.
Kikundi kwa sasa kimeanza kutoa marejesho kiasi cha shilingi 833,333.00/= kwa mwezi mkopo ambao hutolewa bila riba.
SOKO LA BIDHAA LAONGEZEKA
Kikundi kimefanikiwa kuliteka soko kwa kufanikiwa kusambaza bidhaa zao katika karibu shule zote katika wilaya ya Rungwe, Maduka ya viatu katika wilaya ya Kyela, Rungwe, Busokelo na Mbeya mjini.
KIKUNDI CHAJITANGAZA KITAIFA
Kikundi kimefanikiwa kushiriki maonesho ya biashara Sabasaba ambayo mwaka huu kitaifa yanafanyika jijini Dar es salaam. Pia wanajitangaza kwa njia ya mtandao kupitia google play store "Bam leather products" na you tube chanel pia.
Tukuyu Mjini-Mkabala na Benki ya NMB
Sanduku la Posta: Box 148
Simu: 025 255 2586
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: ded@rungwedc.go.tz
Haki Miliki ©2021 GWF. Haki Zimehifadhiwa