SHULE YA SEKONDARI UFUNDI KUPEWA JINA LA RENATUS MCHAU
Baraza la Madiwani kwa robo ya nne Mwaka wa fedha 2023/24 limeazimia shule mpya ya Ufundi inayotarajiwa kujengwa katika kata ya Kisondela kuitwa na kusajiliwa kwa jina la Renatus Mchau ikiwa ni juhudi na mchango wake katika kusimamia na kukuza sekta ya elimu katika wilaya ya Rungwe.
Azimio hilo limefikiwa baada ya Kamati ya Huduma za Jamii chini ya Mwenyekiti wake Mhe.Emmy Maseta kuliomba Baraza hili kupokea pendekezo na kuidhinisha jina la shule hii tarajiwa kusajiliwa kwa jina la Renatus Mchau.
Renatus Mchau ni Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Rungwe .
Jumla ya Shilingi millioni 500 zimetolewa na serikali inayoongozwa na Dkt Samia Suluhu Hassan kwa ajili ya Ujenzi wa shule hii ya Ufundi ambayo inatarajiwa kujengwa katika kata ya Kisondela.
Mhe Maseta amelieleza Baraza kuwa tangu Mkurugenzi Mchau aanze kazi katika wilaya ya Rungwe imeshuhudiwa miradi mingi ya Elimu na Afya inakamilika kwa wakati hatua iliyoongeza upatikanaji wa huduma karibu na Wananchi.
Aidha kutokana na Ubora ya miundombinu ya elimu kwa sasa ufaulu umepanda kwa mitihani ya taifa ambapo kwa elimu ya Msingi na Sekondari ufaulu umefikia asilimia 94 -100%
Pamoja na hayo Matokeo ya kidato cha sita 2024 imeshuhudiwa daraja la nne na sifuri likitupiliwa mbali hatua iliyotokana na Mchau kusimamia upatikanaji wa vifaa vya kufundishia, motisha kwa walimu, udhibiti wa nidhamu na uboreshaji wa mazingira ya kusomea na kujifunzia.
Renatus Mchau alianza kuwatumikia wakazi wa wilaya ya Rungwe mwaka 2021 akitokea katika Halmashauri ya Kilwa ambako pia alihudumu katika nafasi hii aliyonayo sasa.
Jumla ya shule Mpya 7 za sekondari zimejengwa katika kipindi chake ambazo ni (Kyobo, Isaka, Msasani, Kikota, Lupepo, Isaka na Lukata) na Shule za Msingi 4 ambazo ni Chifu Mwanjali, Kibumbe, Ushirika na Umoja. Vituo vya afya (8) ni pamoja na Ndanto, Iponjola, Kyimo, Masebe, Malindo, Kinyala, Masoko, Kiwira
Zaidi ya hayo Mchau amefanikisha ujenzi wa Stendi mpya ya Mabasi katika Mji wa Tukuyu kwa kiwango cha Paving Blocks na Zege, Ununuzi wa Gari jipya la Taka na na dogo kwa ajili ya shughuli za Utawala pamoja uanzishwaji wa Kituo (Packhouse) jumuishi cha Mazao ya Matunda (Parachichi) katika kata ya Nkunga ambapo ujenzi wake unatarajiwa kuanza hivi karibuni. Ujenzi wa soko la Kisasa la ndizi katika kata ya Kiwira (Karasha) nao unatarajiwa kuanza hivi karibuni mara taratibu zitakapokamilika.
Katika hatua nyingine katika kipindi chake Mchau amefanikisha ukusanyaji wa mapato ya ndani kutoka Billion 5.3 Mwaka 2021 Mpaka kufikia Bilioni 7.4 Mwaka huu 2024 hatua iliyosaidia utekelezaji wa miradi mbalimbali ya afya,elimu, Usafirishaji, Motisha kwa watumishi pamoja na ununuzi wa vitendea kazi mbalimbali vya serikali. Baadhi ya miradi iliyotekelezwa kwa mapato ya ndani ni pamoja na ujenzi wa shule mpya ya Umoja na Ushirika, Zahanati ya Lufumbi pamoja na kituo cha afya Kinyala, Malindo , Masebe pamoja na ujenzi wa stendi ya mji wa Tukuyu.
Tukuyu Mjini-Mkabala na Benki ya NMB
Sanduku la Posta: Box 148
Simu: 025 255 2586
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: ded@rungwedc.go.tz
Haki Miliki ©2021 GWF. Haki Zimehifadhiwa