Shule mpya ya Sekondari Kikota-Lubwe iliyopo kata ya kiwira inatarajia kuanza hivi karibuni.Mapema kamati ya Siasa pamoja na Kamati ya Ulinzi na Usalama Wilaya ya Rungwe imekagua ujenzi wa shule hiyo na kuridhishwa na kasi pamoja na viwango vya ujenzi wa majengo ya vyumba sita vya madarasa vinavyotekelezwa chini ya mpango wa Uviko 19.
Vyumba hivyo vitagharimu kiasi cha shilingi Million 120 mara vitakapokamilika hii ikiwa ni pamoja na meza na viti 300.Mkuu wa wilaya ya Rungwe ambaye pia ni Mwenyekiti wa kamati ya Ulinzi na Usalama Mhe. Dkt. Vicent Anney ameagiza mafundi wanaotekeleza mradi huo kukamilisha ifikapo tarehe 25 mwezi huu ili kuwapa nafasi wanafunzi wa kidato cha kwanza kuanza masomo yao mapema.
Naye Mkurugenzi Mtendaji Halmashauri ya Wilaya ya Rungwe Bwana Renatus Mchau ameagiza uongozi wa kata ya Kiwira kuanza kuchimba choo cha wanafunzi na watumishi wa shule hiyo ili kutoa nafasi ya kusajiliwa mapema.
Hata hivyo Afisa Elimu Sekondari Mwalimu Yona Mwaisaka ametaja kuwa wanafunzi watakao jiunga na Shule hiyo katika hatua ya awali watatoka katika shule ya sekondari Kiwira pamoja na Mpandapanda kipaumbele kikiwa ni kwa wanafunzi wanaotoka shule za msingi zilizo karibu na shule hii ikiwa ni hatua nzuri ya kuwapunguzia wanafunzi kutembea umbali mrefu kufuata huduma hii ya elimu.
Katika hatua nyingine Afisa Mtendaji wa Kata ya Kiwira Bwana Noel Mng'ong'o ameeleza kuwa uongozi wa kata hiyo upo mbioni kuanza ujenzi wa Daharia/ Hostel ya shule hiyo mara baada ya kumaliza ujenzi wa Vyumba Saba vinavyotekelezwa na vijiji vinavyounda kata hiyo.
Ujenzi wa Hostel itakuwa ni Ufumbuzi kwa wanafunzi wanaotoka mbali na shule hiyo sambamba na kupandisha kiwango cha ufaulu.
Ambokile Mwaiswelo Mkazi wa kijiji cha Kikota ameishukuru serikali kwa kuwajengea shule hiyo kwani inaenda kutatua changamoto ya watoto wake wawili wanaofuata huduma ya elimu takribani Kilometa saba katika shule ya Sekondari Ukukwe iliyopo kando ya Mlima Rungwe huku Mtoto mwingine akiwa amefaulu kujiunga na kidato cha kwanza mwakani.
Hata hivyo Amina Mwakyoma Mhitimu wa elimu ya Msingi Kikota mwaka huu anashukuru kwa Serikali kumwaga fedha za kutosha katika shule hiyo Mpya kwani itamsaidia kusoma katika mazingira ya karibu na hivyo kuondokana na kadhia ya kwenda katika shule ya Sekondari Kiwira/ Mpandapanda/ Ukukwe ambapo wakati wa mvua nyingi na umbali mrefu wanafunzi hukatiza masomo yao na hivyo kuacha shule kabisa.
Tukuyu Mjini-Mkabala na Benki ya NMB
Sanduku la Posta: Box 148
Simu: 025 255 2586
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: ded@rungwedc.go.tz
Haki Miliki ©2021 GWF. Haki Zimehifadhiwa