RUNGWE KITOVU CHA ELIMU MKOA WA MBEYA
Kikao cha tathimini ya matokeo ya mitihani ya kumaliza elimu ya msingi na sekondari imeitaja wilaya ya Rungwe kuwa wilaya pekee ambayo imeendelea kufanya vizuri kwa miaka mingi mfululizo kati ya Halmashauri 07 zinazounda mkoa wa Mbeya.
Halmshauri zingine ni Kyela, Mbeya jiji, Mbeya vijijini, Busokelo, Chunya na Mbarali.
Tathimini hii imewakutanisha walimu wakuu wote, Wakuu wa shule za sekondari, Waratibu wa elimu kata, Watendaji wa kata zote na Tarafa mkoa wa Mbeya
Kikao hicho kimefanyika tarehe 11.03.2022 Katika ukumbi wa shule ya Sekondari St. Marys jijini Mbeya chini ya Mwenyekiti wake Mkuu wa mkoa wa Mbeya Mhe.Juma Homera huku akiielezea Wilaya ya Rungwe kuwa kila kundi la Watahiniwa imekuwa kinara kwa kutoa watahiniwa wengi huku Halmashauri zingine zikiwa katika nafasi zisizoridhisha.
Mathalani katika Matokeo ya mtihani wa utamilifu kidato cha sita (mock) uliofanyika mwezi February mwaka huu Halmashauri ya wilaya ya Rungwe imeshika nafasi ya kwanza kati ya Halmashauri saba zinazounda mkoa wa Mbeya zikiongozwa na Shule ya sekondari Isongole na Tukuyu.
katika matokeo ya mtihani wa taifa wa kidato cha sita mwaka 2021 shule ya sekondari Tukuyu na Isongole ziliingia katika shule kumi bora sambamba na Mwakaleli na Lufilyo.
Aidha katika matokeo ya mtihani wa kidato cha nne 2021 Halmashauri ya wilaya ya Rungwe ilishika nafasi ya pili nyuma ya Mbeya jiji kwa GPA YA 3.5 huku shule ya sekondari Kayuki, Tukuyu, Bulyaga God'sbridge, Lutengano, zikifanya vizuri
Hata hivyo Rungwe imeshika nafasi ya pili katika matokeo ya Darasa la saba kwa kufaulisha kwa asilimia 90.6% ambapo kata ya Kiwira imetajwa kuwa mfano kwa matokeo mazuri sambamba na kata ya Mafyeko iliyopo wilayani Chunya na Sisimba ya Jiji la Mbeya. Shule ya Mpandapanda na Kiwira ndizo zilizofanya vizuri katika kata ya Kiwira. Shule zingine ni Nuru, God'sbridge, Kellys na Kisa Eng medium.
katika mtihani wa darasa la nne Halmashauri ya Rungwe pia imeshika nafasi ya pili kimkoa huku kata ya Bagamoyo na Mpuguso na Kawetele zikiingia katika kata kumi bora kwa ufaulishaji wa mtihani huo katika Mkoa wa Mbeya.
Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Mhe. Juma Homera amezitaja mbinu za kufuata ili kupanua wigo wa ufaulu kuwa ni pamoja na Kuhakikisha kila shule inatoa chakula cha mchana kwa wanafunzi na walimu.
Kuhakikisha michezo inaendelezwa ili kuongeza uchangamshi kwa wanafunzi.
Kila sekondari kuwa na Hostel ili kuwapunguzia kutembea umbali mrefu na hivyo kuwaepusha na vihatarishi vya matokeo mazuri kama mimba, utoro nakadharika
Kuhakikisha kila Halmashauri inabuni tozo katika mazao yanayozalishwa ili kutunisha mfuko wa elimu na hivyo kuboresha miundombinu ya kusomea na kujifunzia. Akitolea tozo ya Matunda ya parachichi na Kakao inayotekelezwa katika wilaya ya Rungwe.
KWA NINI UWEKEZAJI WA ELIMU RUNGWE UNAWEZEKANA
1. Mipango thabiti ya viongozi na walimu inayowekwa na kutekelezwa kwa vitendo.
2. Hali ya hewa nzuri yenye baridi ya wastani inampa nafasi mwanafunzi kusoma kwa utulivu na umakini.
3. Kihistoria Rungwe ndiyo wilaya yenye shule kongwe zaidi katika mkoa wa Mbeya na Tanzania kwa Ujumla kama Tukuyu, Magereza, Bulyaga, Lupepo, Kilimani, Ibungu, Kapugi nakadhalika na hivyo kuwa kitovu cha elimu kimkoa.
4. Wilaya ya Rungwe ndiyo ina mlima mrefu zaidi nyanda za juu kusini (Mlima Rungwe) na watatu kwa urefu nchini Tanzania hivyo kuwa eneo ambalo wanafunzi wake wanasoma kwa vitendo na kuona uhalisia wa vivutio vingine kama maziwa ya kivolkano kama Ngosi, kisiba, Kyungululu, Ikapu, na ndwati. Maporomoko ya Kaporogwe, Malamba, Mwandambo, kapiki na Malasusa. Majengo ya kale ya Kisiba, Kanseli, Rungwe mission, Kisa na Tukuyu mjini. Nyumba ya Makumbusho ya kabila la Wanyakyusa na wandali iliyopo Rungwe mission. Pamoja na kambi ya uvuvi iliyopo kata ya Isongole iliyojengwa na Wajerumani.
Rungwe ndiyo wilaya pekee mkoa wa Mbeya yenye vivutio vingi vya utalii.
5. Rungwe ina mtandao mkubwa wa barabara zinazofkika kiurahisi kila kona na kuwa kona pekee inayoleta watu katika mikoa yote kwa njia ya mabasi na magari binafsi. Hivyo ukiwekeza katika elimu una nafasi ya kupata wanafunzi nchi nzima.
6. Rungwe inazalisha chakula cha kutosha kwa mwaka mzima na hivyo kuwa wilaya pekee ambayo utapiamlo na udumavu upo kwa kiwango cha chini sana.
7. Mlima Rungwe unasaidia upatikanaji wa Maji kila kona na hivyo wanafunzi kupata maji ya uhakika. Kupitia mradi wa REA vijiji vingi sasa vimeunganishwa na nishati ya umeme.
8. Halmashauri ya Wilaya ya Rungwe ina vituo vya afya vinne vinavyofanya kazi huku vingine vitatu vikiwa katika hatua ya ujenzi/ umaliziaji, zahanati karibu vijji vyote, Hospitali ya Wilaya Tukuyu na Igogwe mission. Hali hii inampa nafasi mwanafunzi kupata huduma ya matibabu kwa ukaribu zaidi.
Tukuyu Mjini-Mkabala na Benki ya NMB
Sanduku la Posta: Box 148
Simu: 025 255 2586
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: ded@rungwedc.go.tz
Haki Miliki ©2021 GWF. Haki Zimehifadhiwa