Mkuu wa mkoa wa Mbeya Mheshimiwa Juma zuberi Homera amekabidhi basi la abiria kwa kikundi cha wanawake Miujiza kilichopo Katumba kata ya Ibighi.
Tukio hilo limefanyika leo katika kilele cha maadhimisho ya siku ya Wanawake duniani ambapo kimkoa yamefanyika wilayani Rungwe katika stendi ya daladala Tukuyu Mjini.
Basi hilo limekopeshwa kwa kikundi hicho kama mkopo unaotolewa na Halmashauri ikiwa ni asilimia 10% ya mapato yake ya ndani ambapo pamoja na hayo jumla ya vikundi 15 vimekopeshwa mkopo wenye thamani ya shilingi million 186 kwa robo ya pili.
Katika maadhimisho hayo Mhe.Homera ameishukuru Halmashauri kwa kuendelea kutoa mikopo kwa vikundi mbalimbali kwa kila robo na kuwa hali hiyo itaenda kuinua kipato cha kaya na jamii kwa ujumla.
Hata hivyo ameviagiza vikundi hivyo kuendelea kurejesha mikopo hiyo kwa wakati kwani hutolewa bila riba na hulenga kuwafikia walengwa wengi zaidi.
Katika hatua nyingine Mhe.Homera ameikumbusha jamii kuendelea kulinda haki za wanawake na watoto ili kuleta ustawi bora katika jamii.
Amesema jamii yoyote ili iendelee inahitaji mazingira mazuri yaliyoboreshwa kwa ajili ya Wanawake na Watoto hivyo kila mtu hana budi kupinga vitendo vya kikatili na unyanyasaji vinavyoendelea dhidi ya makundi hayo katika maeneo yetu.
Maadhimisho hayo yaliyokuwa na kauli mbiu iliyolenga kuwajengea uwezo wanawake katika sekta ya teknolojia yameshuhudiwa na maandamano ya wanawake kutoka wilaya zote, vikundi vya burudani, maonesho ya bidhaa za wajasiriamali, ushauri wa kisheria pamoja na upimaji wa afya ya binadamu.
Tukuyu Mjini-Mkabala na Benki ya NMB
Sanduku la Posta: Box 148
Simu: 025 255 2586
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: ded@rungwedc.go.tz
Haki Miliki ©2021 GWF. Haki Zimehifadhiwa