Nchi ya Malawi imeendelea kutumia Reli ya TAZARA ikiwa ni njia pekee ya kusafirisha mizigo ya nchi hiyo sambamba na kupunguza uharibifu wa barabara kwa kupakia mizigo inayozidi uwezo.
Rai hiyo imetolewa na Naibu waziri wa Ujenzi na Uchukuzi nchini Malawi Mhe. Nancy Chaola Mdooka (MB) wakati akizungumza na Watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Rungwe alipofanya ziara fupi leo tarehe 12. 10 2021 ambapo pamoja na maeneo mengine ametembelea Bandari ya Kiwira Ziwa Nyasa, na Bandari kavu ya Malawi Cargo iliyopo Iyunga jijini Mbeya.
Mhe. Chaoka amesema kuwa kwa sasa nchi hiyo inategemea ndizi kutoka nchini Tanzania hususani katika Wilaya ya Rungwe baada ya migomba nchini kwake kukumbwa na ugonjwa wa mnyauko hivyo hii ni fursa pekee kwa wakulima na wafanyabiashara kuchangamkia soko hilo.
Aidha amesema kuwa wakazi wa nchi ya Malawi wapo tayari kushirikiana katika sekta mbalimbali hivyo hatuna budi kuendelea kushikamana na kuimarisha uwekezaji kwa manufaa ya watu wetu.
Akimkaribisha Waziri huyo Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Mhe. Juma Homera ameutaja Mkoa huu kuwa lango imara kwa Uchumi wa nchi ya Malawi hivyo uwepo wa Uwanja wa ndege wa Songwe, Bandari ya Kiwira, Reli ya Tazara na Barabara kuu kuwa kichocheo cha uchumi wa nchi hiyo.
Amesema kuwa takribani wakazi wengi wa nchi ya Malawi wanatumia uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Songwe ikiwa ni njia ya kusafiria kwenda nje ya nchi sambamba na kutumia reli na barabara zetu kusafirishia mizigo yao.
“Niwaombe sana mtumie miundombinu yetu na mje muwekeze katika viwanda vya uongezaji thamani wa mazao yetu kama Ndizi, Viazi Mviringo, kahawa, chai na parachichi ili wakazi wa wilaya ya Rungwe wapate soko la uhakika la mazao yao” amesisitiza
Pamoja na hayo Mhe. Homera ameomba lugha ya Kiswahili kuendelea kutumika katika nchi hizo mbili likiwa ni daraja muhimu la mawasiliano katika biashara, utalii, kilimo, elimu na shughuli nyingine nyingi.
Hata hivyo Mkuu wa Wilaya ya Rungwe Mhe. Dk Vicent Anney ameitaja wilaya hii kama kitovu cha uzalishaji na uwekezaji wa shughuli mbalimbali za kiuchumi na kuwa mazingira tayari yameandaliwa kwa kuwekeza mitaji na amealika Watanzania na Wageni mbalimbali kuja kuwekeza katika wilaya hii.
Tukuyu Mjini-Mkabala na Benki ya NMB
Sanduku la Posta: Box 148
Simu: 025 255 2586
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: ded@rungwedc.go.tz
Haki Miliki ©2021 GWF. Haki Zimehifadhiwa