Jumla ya shilingi million 210,500,000/= zimetolewa na Halmashauri ya wilaya ya Rungwe leo tarehe 30.6.2021 Kwa vikundi 31 vya Wanawake, Vijana na Watu kwenye ulemavu ikiwa ni asilimia kumi ya mapato yake ya ndani ambapo mkopo huu hutolewa bila riba.
Bwana Omary Mungi ni Afisa Maendeleo ya Jamii Wilaya ambapo amearifu kuwa Kwa mwaka huu wa fedha 2020/21unaoishia June 30 mwaka huu, jumla ya shilingi million 848,500,000/= zimetolewa Kwa vikundi 123 huku ukinufaisha vikundi vya Wanawake 79, Vijana 40 na watu wenye ulemavu vikundi 04. Mikopo hii hujumuisha mchango wa Halmashauri na marejesho kutoka Kwa wanufaika.
Akitoa mikopo hiyo Leo mapema Mwenyekiti Halmashauri ya Wilaya ya Rungwe Mhe. Mpokigwa Mwankuga ambaye pia alikuwa mgeni rasmi katika hafla hiyo, ameomba wanufaika kuwa wabunifu ili kuwasaidia kuingia katika soko la ushindani Kwa kuzalisha bidhaa zenye tija kwa jamii.
" Jitahidini kuzalisha kwa tija na kubuni vifungashio vitakavyo mteka mnunuzi na kumfanya avutiwe na bidhaa yako" Ameongeza Mhe. Mwankuga
Aidha ameonya vikundi vyote kutumia mikopo hiyo Kwa malengo yaliyokusudiwa ili kusaidia kuinua kipato cha kikundi, kaya na taifa Kwa ujumla na hivyo kusaidia kuvinufaisha vikundi vingine vitakavyokopa katika Msimu unaofuata.
" Kuna watu hapa wameshawaambia nyumbani kuwa tumepata fedha hivyo wawe tayari kula nyama na kuvaa nguo nzuri, Niwaonye! Fedha hizi zitumike Kwa malengo yaliyoombewa. Muwe wabunifu kwa kuanzisha vitega uchumi vitakavyosaidia mle nyama siku zote maisha yenu yote na si vinginevyo" Ameonya na kutoa ushauri.
Akimkaribisha Mgeni rasmi Mkurugenzi Mtendaji Halmashauri ya wilaya ya Rungwe Bi. Loema Peter amesema kuwa Halmashauri imeendelea kutoa mikopo hiyo ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa ilani ya chama tawala "CCM" na kuomba wakazi wa wilaya ya Rungwe kuendelea kulipa kodi ili kuijengea mazingira mazuri serikali yao kutoa mikopo yenye thamani kubwa na hivyo kuwafikia wakazi wengi zaidi.
" Niombe wakazi wenzangu tulipe kodi na tuhakikishe tunazuia mianya yote inayopelekea ukwepaji wa kodi hii itasaidia kuinua uchumi wetu na serikali kutoa huduma stahiki kwa umma".
Hafla hiyo imehudhuriwa na katibu wa Mbunge Jimbo la Rungwe Bwana Gabriel Mwakagenda ambapo amehamasisha wanufaika kuwa mabalozi kwa watu wengine huku wakieleza namna serikali yao inavyowajali watu wake kwa kuwapatia mikopo isiyo na riba ambayo kwa muda mrefu imebadilisha maisha ya Watanzania wengi.
"Kuweni waaminifu kurejesha mikopo kama serikali ilivyowaamini na kuwakabidhi mikopo hii. Nendeni mkaitangaze vizuri serikali yenu kwa mema iliyowatendea" Amemaliza bwana Mwakagenda
Tukuyu Mjini-Mkabala na Benki ya NMB
Sanduku la Posta: Box 148
Simu: 025 255 2586
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: ded@rungwedc.go.tz
Haki Miliki ©2021 GWF. Haki Zimehifadhiwa