MHE. HOMERA AFANYA ZIARA KIJIJI CHA LUFUMBI
Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Mhe. Juma Homera amefanya ziara Leo alasiri tarehe 20 .08.2022 katika Kijiji Cha Lufumbi kata ya Masoko.
Akihutubia umati mkubwa uliojitokeza kumlaki katika Kijiji hicho , Mhe. Homera amesisitiza wakazi wa kata hiyo na Mkoa kwa ujumla kujitokeza na kushiriki zoezi la Sensa ya watu ya Makazi linalotarajia kufanyika siku ya jumanne agosti 23, 2022..
Ametaja mambo ya kuzingatia siku hiyo kuwa ni pamoja na kutoa takwimu sahihi za umri, elimu, jinsi, hali ya ndoa, umiliki wa kitambulisho Cha taifa, shughuli za kiuchumi ambapo takwimu hizo zitatolewa kwa karani wa sensa dhidi ya watu wote waliolala katika kaya husika usiku wa kuamkia siku ya Sensa.
Aidha Mkuu wa Mkoa ameahidi kutoa bati kwa ajili ya ukamilishaji wa Ofisi ya Kijiji Cha Lufumbi ambapo kumalizika kwake kutaimarisha na kurahisisha shughuli za utawala bora Kijiji hapo .
Wakati huo huo Mkuu wa Wilaya ya Rungwe Mhe Dkt. Vicent Anney ameahidi kutoa jumla ya mifuko 20 ya saruji huku Ofisi ya Mbunge Jimbo la Rungwe ikiahidi kutoa jumla ya mifuko 100 ya saruji ikiwa ni jitihada ya kuunga mkono nguvu za wananchi Katika ujenzi wa Ofisi hiyo.
Katika hatua nyingine Mhe. Homera amearifu kuwa serikali ipo Mbioni kuanza ujenzi wa Chuo Cha ufundi- VETA katika Halmashauri ya Wilaya ya Rungwe ikiwa ni ahadi ya Mhe. Rais alipofanya ziara mapema Mwezi huu huku tayari akiwa ametoa jumla ya shilingi Million 10 kwa ajili ya ujenzi wa kituo cha afya katika kata ya Kiwira.
Mhe Homera ameipongeza kamati ya Ulinzi na Usalama wilaya Rungwe, Baraza la Madiwani, Menejimenti, Watumishi na Wakazi wote Wilayani Rungwe kwa kutekelezwa ipasavyo na kwa wakati miradi ya Maendeleo ambapo ameitaja miradi hiyo kuwa ni pamoja na uanzishwaji wa shule mpya nne za Sekondari na ujenzi wa Ofisi 30 za walimu kwa fedha za UVIKO 19.
Wakati huhuo Mkurugenzi Mtendaji Halmashauri ya Wilaya ya Rungwe Bwana Renatus Mchau amearifu kuwa Halmashauri imetenga jumla ya shilingi Million 20 kwa ajili ya ukamilishaji wa zahanati ya Kijiji hicho na kueleza kuwa baada ya wiki mbili fedha hizo zitakuwa zimepelekwa katika Kijiji hicho na hivyo kuwezesha wakazi wa kata hiyo kupata huduma ya matibabu karibu na kaya zao.
Kata ya Masoko inapatikana katika barabara Tukuyu- Busokelo ni maarufu kwa kilimo Cha ndizi, tangawizi, parachichi, iliki, kahawa, miti ya mbao na ufugaji.
Katika mwaka wa fedha uliopita Halmashauri ya Rungwe ilikusanya mapato yake ya ndani kwa asilimia 104 ambapo mapato ya Kikata kata ya Masoko imekusanya mapato kwa asilimia 120 ikishika na nafasi ya pili chini ya kata ya Ilima hali inayotajwa kuongeza fursa kwa Serikali kutekelezwa majukumu yake kwa wananchi wake kwa urahisi.
Tukuyu Mjini-Mkabala na Benki ya NMB
Sanduku la Posta: Box 148
Simu: 025 255 2586
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: ded@rungwedc.go.tz
Haki Miliki ©2021 GWF. Haki Zimehifadhiwa