Hafla ya kuwapongeza wanafunzi wa shule ya Sekondari wasichana Kayuki pamoja na uongozi wa shule hiyo umefanyika leo Jumapili tarehe 20.03.2022 alasiri katika Ukumbi wa Shule hiyo.
Pongezi hizo zimeandaliwa na Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji Halmashauri ya wilaya ya Rungwe kufuatia shule hiyo kuwa miongoni mwa Shule kumi bora za wananchi kitaifa katika matokeo ya mtihani wa kidato cha nne mwaka 2021 na kupewa cheti,Kikombe na Waziri wa TAMISEMI.
Shule hii imekuwa ikifanya vizuri katika mitihani yote kitaifa kwa miaka mingi mfululizo na hivyo kuwa moja ya shule bora zaidi Nyanda za juu kusini na Taifa kwa Ujumla.
Pamoja na mambo Mkurugenzi mengine ameandaa na kushiriki chakula cha mchana kwa wanafunzi na watumishi wa shule hiyo.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Rungwe Mhe. Mpokigwa Mwankuga ndiye alikuwa mgeni rasmi ambapo amewaomba wanafunzi wa shule hiyo kusoma kwa bidii na hivyo kuendelea kuwa kioo cha Halmashauri ya Rungwe sambamba na kuandaliwa kuwa viongozi bora nchini.
Aidha ameziagiza shule nyingine katika Halmashauri kuiga mfano wa shule hii kwa kufanya hivyo itasaidia kuinua kiwango cha taluma, maarifa na ujuzi sanjari na kuiweka Rungwe katika ramani bora ya elimu nchini.
Wakati huohuo Mkurugenzi Mtendaji Halmashauri ya Wilaya ya Rungwe Bwana Renatus Mchau amearifu kuwa Shule ya sekondari Bujinga na Tukuyu zimekuwa zikipanda kitaluma na hivyo kuwa katika hatua ya kiushidani ambapo katika mitihani ya kidato cha nne na pili kwa vipindi tofauti zimeonesha mafanikio mazuri.
Aidha ameushukuru uongozi wa shule hiyo kwa kusimamia nidhamu na taluma kwa shule hiyo na kuifanya kuwa katika nafasi ya kumi bora kitaifa.
Hata hivyo ameeleza kuwa serikali mara itakapopata fedha inatarajia kuikarabati shule hiyo na kuwa katika mazingira nadhifu ya kusomea na kujifunzia.
Naye Mkuu wa Shule hiyo Mwalimu Sarufu ameshukuru Menejimenti ya Halmashauri ya Wilaya ya Rungwe kwa kuandaa hafla hiyo na kuahidi kudumisha ufaulu sambamba kuhakikisha wanafunzi wa kidato cha sita wanaotarajia kuanza mtihani wa mwezi mei mwaka huu wanafaulu kwa daraja la juu na hivyo kuwa katika nafasi bora shindani kitaifa.
Wageni wengine waliohudhuria na kutoa nasaha (motivation speaker) ni pamoja na Mwenyekiti wa kamati ya Elimu na Huduma za Jamii Mhe. Emmy Maseta, Meneja wa Benki ya CRDB tawi la Rungwe Bi Devotha Mshanga, Hakimu Wilaya ya Rungwe, Katibu wa TSC- Tume ya Walimu wilaya, na Makamu wa bodi ya shule hiyo wote wanawake.
Tukuyu Mjini-Mkabala na Benki ya NMB
Sanduku la Posta: Box 148
Simu: 025 255 2586
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: ded@rungwedc.go.tz
Haki Miliki ©2021 GWF. Haki Zimehifadhiwa