Halmashauri ya Wilaya ya Rungwe kwa Kushirikiana na kampuni ya Bioland inayojihusisha na ununuzi wa zao la Kakao kupitia mradi wa Cocoa for schools wamejenga na kukarabati zaidi ya vyumba 36 vya madarasa katika shule za msingi zilizopo katika kata ya Kisiba, Masukulu na Matwebe.
Kampuni hii hufanya hivyo kama rejesho kwa wakulima baada ya kupata faida (Corpoarate social rensponsibility ).
Shule za msingi zilizonufaika ni pamoja na Mbaka, Masoko, Busilya, Isabula, Ikomelo, Matwebe, Mpelangwasi, Kikole na Njugilo
Akizundua madarasa hayo kwa nyakati tofauti Mkuu wa wilaya ya Rungwe Mhe.Dkt Vicent Anney ameagiza uongozi wa shule hizo kuendelea kuyatunza ili yavifaidishe vizazi vijavyo huku kampuni ya Bioland ikipanua misaada zaidi kwa kuhusisha shule za Sekondari pamoja na vifaa vya kufundishia.
Katika kipindi cha miezi mitatu (Januari- Marchi 2022) iliyopita Katika Halmashauri ya ya Wilaya ya Rungwe jumla ya kilo 31,290 zimeuzwa kupitia mnada wa Ntaba na Kyela na wakulima kujipatia jumla ya shilingi 136,644,410/= fedha ambazo zimebadilisha sura ya uchumi wa wakazi wa kata hizi.
Ukanda huu umefunguka sana kutokana na umuhimu wa zao hili na shule zinapendeza sana.Kupitia vikao mbalimbali vya wadau wa zao la kakao wakulima walikubaliana kukatwa shilingi 20 kwa kila kilo ikiwa ni sehemu ya kutunisha mfuko wa elimu pamoja na huduma zingine za kijamii kama maji na afya.
ZAO LA KAKAO
Kutokana na kuongezeka kwa mahitaji ya chokoleti duniani, wakulima wa wakazi wa wilaya ya Rungwe wameanzaza kufaidika na soko la kakao baada ya kuanza kujengewa uwezo wa kulima kisasa ili kuongeza uzalishaji.
Shirika la Kimataifa la Kakao (ICCO) linaripoti kuwa karibu asilimia 90 ya chokoleti yoteinayotengenezwa duniani hutumiwa na nchi zilizoendelea zikiwemo za Ulaya, Asia na Amerika ya Kusini, huku asilimia 70 ya chokoleti hiyo hutokana na kakao inayozalishwa barani Afrika.
Katika bara la Afrika nchi ya Ivory Coast, Ghana, Nigeria na Cameroon ndio wazalishaji wakubwa wa kakao barani Afrika licha ya kuwepo maeneo mengine ya Magharibi na Afrika ya Kati ambayo mpaka sasa hayajatumia vizuri fursa ya kulima zao hilo.
Nchini Tanzania, zao hilo hulimwa katika Wilaya za Kyela na Rungwe mkoa wa Mbeya ambapo huzalisha zaidi ya asilimia 80 ya kakao yote nchini.Katika Halmashauri ya wilaya ya Rungwe hulimwa zaidi katika kata ya Matwebe, Masukulu, Bujela, Kisiba na Masoko.
Kwa upande wa Busokelo zao hili hulimwa Kwa wingi katika maeneo ya Ntaba, Mbambo, Kambasegela, Lufiliyo, Itete, Kisegese Ntapisi na mengine mengi.Maeneo mengine nchini Tanzania ni pamoja na wilaya ya Ifakara, Turiani na Kilosa Morogoro na Maramba-Tanga na mchakato wa kulima zao katika mkoa wa Kigoma unaendelea.
Mti wa kakao asili yake sio Tanzania, uliingizwa barani Afrika zaidi ya miaka 100 iliyopita ukitokea Amerika ya Kusini, lakini sasa Afrika ndio mzalishaji mkubwa duniani.
Tanzania inaweza kufaidika na zao hilo kwasababu ni nchi pekee ya Afrika Mashariki ambayo hali ya hewa inaruhusu kulima zao hilo katika baadhi ya maeneo nchini.Inakadiriwa kuwa Tanzania huzalisha zaidi ya tani 7,000 kila mwaka hali ambayo inahitaji msukumo wa ziada kwa mkulima mmojammoja kulingana na mahitaji makubwa ya zao hili katika soko la Duniani.
.Baada ya miaka 4 au 5 toka kupandwa Mti wa kakao hukomaa na kuanza kuzaa mbegu ambazo huwa ndani ya kokwa (pods) .
Kwa wastani mti mmoja wa kakao unazalisha matunda 20 hadi 30 wakati wa uvunaji.Kila kokwa hubeba mbegu 20 hadi 50 ambazo hujulikana kama mbegu za kakao.Hii ni sawa na kilo 3-5kgs kwa kila mti wenye umri wa miaka 3-6 . Mti wenye umri kuanzia miaka 9 hadi 15 huzaa kilo 10 hadi 15kgs kwa msimu ukitunzwa vizuri.
Baada ya kokwa kukomaa huvunwa na kupasuliwa na kuwekwa kwenye chombo maalumu ili zichachuke kwa siku 3 hadi 5 . Mbegu hizo hukaushwa, huoshwa, hubanikwa mchakato mchakato unaosaidia kupata malighafi ya kutengeneza bidhaa mbalimbali ikiwemo chokoleti, vinywaji dawa za binadamu na vipodozi.Bei ya kakao kwa msimu mkuu uliopita ilikuwa shilingi 3500/= hadi kufikia 4200/= kwa kilo hali iliyochangia kuinua kipato cha wakulima ikiwa ni pamoja na kumudu kunilipia huduma mbalilbali kama matibabu, elimu, maji, umeme, chakula pamoja na ujenzi wa nyumba za kisasa.
Anyigulile Mwakasege mkazi wa kijiji cha Mpelangwasi kata ya Matwebe amekiona kilimo hiki kama mkombozi wa maisha yake kwa kuwa kinampa fursa ya kuwa na kipato katika msimu wote wa mwaka na hivyo kumudu kuwa na uhakika wa kuihudumia familia yake.
Kilimo cha kokoa kinatunza unyevunyevu na kuongeza afya ya udongo kutokana na majani yake kuanguka kwa wingi chini ya shina hali inayompa furaha bwana Amosi Mwanguku Mkazi wa Masukulu kwani tangia apande shamba lake halina gharama ya parizi zaidi ya shughuli ya kupogolea maatawi yasiyofaa na hivyo muda mwingi anajihusisha na shughuli za mazao ya chakula.
Matawi ya mikokoa hutumika kama kivuli hasa msimu wa kiangazi ukingatia zao hili hulimwa maeneo yenye joto la chini kuanzia nyuzi 18-21°C na kiwango cha juu kufikia nyuzi 30-32°C.Uwepo wa barabara ya Tukuyu - Busokelo inayoendelea kujengwa Kwa kiwango cha Lami na ile Landan- Matwebe- Ipande Kyela pamoja na Council - Masukulu inatajwa kuwa kiungo muhimu cha uharakishwaji wa uchavushaji wa uchumi katika ukanda huu kupitia zao hili muhimu.
Ghala kubwa la kukusanyia kokoa linalotarajiwa kujengwa katika kata ya Kisiba litasaidia kuhifadhi zao hili Kwa Msimu wote mfululizo na hivyo kuwa eneo muhimu ( Economic hub) ya uchumi Kwa wakazi wa pembe hii.
IDADI YA MICHE KWA EKARI
Ekari moja ya ukubwa wa shamba la mita 70 kwa 70m Cocoa hupandwa umbali wa mita 3 mche/mti hadi mche/mti na 4m mstari hadi Mstari Kwa ukubwa huu panda miche 410 hadi 500 kwa shamba la ekari moja.
UREFU WA MTI WA KOKOA
Mti wa kakao uliotunzwa vizuri ni mdogo kwa kiasi cha futi 13 hadi 26, matawi yake ni ya kijani ambapo hulimwa maeneo yenye hali ya hewa ya kitropiki.
UTALII WA MAZAO UMEPANUKA WILAYANI RUNGWE
Pamoja na mazao mengine kokoa limekuwa zao lenye mvuto wa pekee kwa wageni wanaotembelea maeneo yanayozalisha zao hili. Watalii wanaotembelea ziwa Kisiba na Maporomoko ya maji Isabula hutumia muda wao kufanya utalii wa matembezi na kufaidika na kivuli murua cha mti wa mikokoa pamoja na kula matunda yake yenye radha nzuri ya sukari. Mazao mengine ni pamoja na Vanila, na Chai na Parachichi.
Tukuyu Mjini-Mkabala na Benki ya NMB
Sanduku la Posta: Box 148
Simu: 025 255 2586
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: ded@rungwedc.go.tz
Haki Miliki ©2021 GWF. Haki Zimehifadhiwa