Halmashauri ya wilaya ya Rungwe ipo mbioni kumaliza Ukarabati na ujenzi wa soko la la kisasa katika eneo la Tandale lililopo kata ya Bulyaga mkabala na uwanja wa mpira ambalo mpaka kumalizika kwake linatarajia kugharimu zaidi ya shilingi million 200.Gharama hizo zitajumuisha ujenzi wa soko hilo jipya, ukarabati wa soko la zamani, miundombinu ya maji safi na taka, umeme, pamoja na barabara.
Mwenyekiti wa kamati ya uwekezaji Halmashauri ya Wilaya ya Rungwe Bwana Omary Mungi ametaja kuwa soko hilo litakuwa na vizimba 120 huku wanufaika wengine wakiandaliwa maeneo kuzunguka soko hilo na hivyo kuwa na jumla ya wanufaika 401.
Amenye Mwaigwisya ameishukuru Serikali kwa kuwajengea soko hilo na kuwa kwa sasa wataepukana na adha ya kunyeshewa na mvua pamoja na usalama wa mali zao.
Aidha bibi Ashura Mwaigwisya amepongeza kwa hatua nzuri iliyofikiwa na kuwa wataendelea kulipa kodi ya serikali ili kutoa fursa ya kuendelea kulikarabati soko hilo mara kwa mara na kutoa huduma zingine.
Soko la Tandale hudumu kwa siku zote saba za wiki pamoja na gulio kwa siku ya jumatatu na alhamisi.Halmashauri ya wilaya ya Rungwe imeendelea na ujenzi pamoja na ukarabarti wa masoko yake mbalimbali ikiwa ni hatua muhimu ya kuboresha mazingira mazuri ya biashara kwa Watanzania.
Masoko hayo ni pamoja na Kiwira, Tukuyu stendi, Mwambenja, Ibililo, Soko la Wamachinga mkabala na Mamlaka ya Mpato Tanzania-(TRA) pamoja na soko la Nzunda ambalo linajengwa na Serikali ya kijiji hicho kwa kutumia mapato yake ya ndani.
Pamoja na hayo Halmashauri ipo mbioni kujenga soko la kimataifa la ndizi katika kijiji cha Kiwira pamoja na viazi katika kijiji cha Mbeye one kata ya Isongole na ghala la kununulia na kukusanyia kakao katika kijiji cha Lwifwa kata ya Kisiba.
Kumalizika kwa masoko haya kutafungua fursa kwa wafanyabiashara kununua bidhaa kwa urahisi, serikali kukusanya mapato yake kwa urahisi sambamba na kuimarisha mifumo ya upatikanaji wa takwimu za mazao ya kilimo.
Tukuyu Mjini-Mkabala na Benki ya NMB
Sanduku la Posta: Box 148
Simu: 025 255 2586
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: ded@rungwedc.go.tz
Haki Miliki ©2021 GWF. Haki Zimehifadhiwa