Wakazi wa wilaya ya Rungwe wamekumbushwa kuendelea kuchangamkia fursa mbalimbali za uwekezaji wa mitaji yao kwani Kwa kufanya hivyo watapata tija na maendeleo lukuki.
Rai hiyo imetolewa na Afisa Tawala wilaya ya Rungwe bwana Aimu Mwandelile wakati akifungua baraza la biashara mapema Leo katika ukumbi wa halmashauri ya wilaya ya Rungwe ( Mwankenja). "Rungwe ina hali ya hewa nzuri rutuba ya udongo na maeneo mengi ya uwekezaji na Kwa kuanzia uwekezaji mkubwa umefanyika katika ziwa masoko/ kisiba ambapo wakazi wa maeneo hayo wameanza kunufaika Kwa kufanya biashara doto kuzunguka eneo la uwekezaji".
Bwana Mwandelile ameongeza kuwa serikali inaendelea kuimarisha miundombinu rafiki kama barabara na umeme ili kuwezesha wafanyabiashara kufanya shughuli zao Kwa ufanisi mkubwa.
Atupele Mwasalemba mkazi wa kijiji cha Ndubi kata ya Kisondela ameunga mkono kauli ya katibu Tawala Kwa kuona namna itakavyo warahisishia kusafirisha mazao ya migomba , kahawa na tangawizi kutoka mashambani kwenda sokoni baada ya barabara ya Masebe- Lutete kukamilika Kwa kiwango cha lami.
Furaha ya Mwasalemba inapewa chapuo na wakazi wa kijiji cha Ilenge kwani uwepo wa umeme wa kutosha na ujenzi wa barabara ya lami kuelekea kiwanda cha Rungwe Avocado inawapa ari ya kuzalisha mazao Kwa tija na kuanzisha viwanda vidogovidogo.
Aidha afisa biashara wilaya bwana Yesaya Mwakisole amewaomba wafanya biashara ndogondogo kutofanya shughuli zao maeneo yasiyoruhusiwa kisheria kwani kufanya hivyo wanahatarisha maisha yao ikiwa ni pamoja na kupoteza mapato ya serikali.
" Utaona siku ya gulio la Tandale wafanyabiashara wanaweka bidhaa zao katikati ya barabara ya Busokelo hii siyo sahihi" Alisisitiza.
Pamoja na hayo wafanyabiashara wamesisitizwa kuendelea kukata leseni na vitambulisho vya ujasiriamali ili kusaidia na kurahisisha shughuli za biashara.
Halmashauri ya wilaya ya Rungwe ina fursa nyingi za uwekekezaji ikiwa ni pamoja na uzalishaji na usafirishaji wa parachichi, ndizi, nanasi, viazi mviringo, chai, kahawa, cocoa vanilla, iliki, tangawizi, maziwa, samaki, na nyama ya ng'ombe. Pia ujenzi wa hotel, campsite katika vivutio vya utalii.
Fursa nyingine ni ujenzi wa viwanda vya kuchakata bidhaa mbalimbali
Baraza la biashara hujumuisha sekta binafsi pamoja uongozi wa umma na Kwa mshikamano huo imesaidia kutatua changamoto mbalimbali za biashara nchini.
Tukuyu Mjini-Mkabala na Benki ya NMB
Sanduku la Posta: Box 148
Simu: 025 255 2586
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: ded@rungwedc.go.tz
Haki Miliki ©2021 GWF. Haki Zimehifadhiwa