DC.HANIU AFANYA ZIARA KATA YA IKUTI
Mkuu wa wilaya ya Rungwe Mhe Jaffar Haniu amefanya ziara katika kata ya Ikuti na kukagua miradi ya maendeleo pamoja na kuzungumza na wakazi wa kata hiyo.
Akikagua ujenzi wa shule mpya ya msingi katika kijiji cha Ikuti pamoja hosteli ya wavulana katika shule ya sekondari Ikuti Kwa nyakati tofauti, Mhe.Haniu amepongeza wakazi wa kata hiyo kwa jitihada wanazozionesha katika kushiriki na kuchangia shughuli za maendeleo na Kuwa hatua hiyo itaharakisha upatikanaji wa maisha bora kuanzia ngazi ya kaya na kata kwa ujumla.
Aidha ameagiza uongozi wa kata hiyo kukamilisha ujenzi wa jengo la mionzi (X-Ray) katika kituo hicho cha afya Ikuti ili kurahisisha upatikanaji wa huduma ya afya kwa ukaribu zaidi.
" Serikali yenu sikivu sana, imeshanunua kifaa hiki muhimu kwa matibabu ya wananchi hivyo siyo vema tukashindwa kukitumia kwa kukosa jengo. Tafadhari tushikamane kukamilisha ujenzi huu" Amesisitiza.
Katika hatua nyingine Mhe. Haniu ameuagiza uongozi wa kata hiyo kuhakikisha unasimamia ipasavyo usomaji wa mapato na matumizi katika vijiji vyote ikiwa ni nyenzo muhimu katika utawala bora na Ushirikishwaji wa wananchi katika kufikia maamuzi ya maendeleo yao.
Aidha ametoa maelekezo kwa wakazi wa kata hiyo na wilaya kwa ujumla kushiriki katika mikutano ya hadhara ,kutoa maoni na kujadiliana bila kuathiri amani na utulivu na Kuwa viongozi wa dini na mila wana nafasi kubwa kutatua changamoto zinazowakabili badala ya kuanzisha na kushiriki katika migogoro mbalimbali.
Wakati huo huo ameagiza wazazi wote katika shule zote zilizopo katika wilaya ya Rungwe kuhakikisha wanachangia chakula shuleni ili kuongeza ufaulu sambamba na kuondoa utapiamlo na udumavu kwa wanafunzi.
Hata hivyo Mhe. Haniu ameeleza Kuwa haya yatawezekana iwapo wakazi wa wilaya ya Rungwe wataendelea kutunza mazingira na kulinda vyanzo vya maji ili kuhakikisha upatikanaji wa mvua na maji unakuwa endelevu mwaka mzima.
Katika ziara hiyo ambayo pia ilihudhuriwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Rungwe Bwana Renatus Mchau ambapo ametaja baadhi ya miradi inayotekelezwa katika kata hiyo Kuwa ni pamoja Ujenzi wa nyumba ya walimu katika shule ya sekondari Kyobo, Ukamilishaji wa nyumba ya watumishi katika zahanati ya Kyobo, Ujenzi wa vyumba viwili pamoja na vyoo katika shule ya msingi Ikuti na Kinyika pamoja na miradi mingine ya maji, umeme na bahrabara inayoondelea.
Tukuyu Mjini-Mkabala na Benki ya NMB
Sanduku la Posta: Box 148
Simu: 025 255 2586
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: ded@rungwedc.go.tz
Haki Miliki ©2021 GWF. Haki Zimehifadhiwa