Baraza la madiwani la kawaida limeketi leo katika Ukumbi wa halmashauri ya wilaya ya Rungwe ambapo pamoja na mambo mengine waheshimiwa madiwani wamepongeza namna halmashauri inavyosimamia miradi mbalimbali huku wakiumulika mradi wa ujenzi na ukarabati wa Shule ya sekondari wavulana Rungwe, pamoja na ujenzi wa jengo la mama na mtoto Hospitali ya wilaya TUKUYU- Makandana.
Aidha mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Rungwe Mhe.Mpokigwa Mwankuga amesisitiza kuwa kwa sasa uchangiaji wa chakula cha mchana kwa wanafunzi wa shule za msingi na sekondari litakuwa ni suala la lazima kwa kila mzazi kushiriki mchango huo ili kuinua kiwango cha taaluma na kutokomeza utapiamlo na udumavu kwa watoto.
Akimkaribisha Mwenyekiti, Kaimu Mkurugezi halmashauri ya wilaya ya Rungwe bwana Castor Makeula amehimiza watendaji wa kata katika maeneo yote kuhakikisha wanarejesha makusanyo yote kwa wakati ili kusaidia halmashauri kutekeleza majukumu yake ikiwa ni pamoja na utekelezaji wa miradi mbalimbali.
Akimwakilisha Mkuu wa wilaya ya Rungwe, Afisa Tawala wilaya bwana Hamimu Mwandelile ameshukuru halmashauri kwa namna inavyobuni vyanzo mbalimbali vya mapato ili kujijengea uwezo imara wa uchumi huku akiangazia mradi wa uendelezaji wa ufukwe wa ziwa kisiba mradi unaotajwa kuinufaisha halmashauri pamoja na wakazi wanaouzunguka.
Akifunga baraza hilo Mhe. Mpogigwa Mwankuga ameomba watendaji pamoja na madiwani kuendelea kushirikiana kwa lengo la kujenga mshikamano imara wenye kuwaletea maendeleo endelevu wananchi na hivyo kutekeleza ilani ya chama cha mapinduzi kwa vitendo na matokeo makubwa.
Tukuyu Mjini-Mkabala na Benki ya NMB
Sanduku la Posta: Box 148
Simu: 025 255 2586
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: ded@rungwedc.go.tz
Haki Miliki ©2021 GWF. Haki Zimehifadhiwa